Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza la Usalama lalaani shambulizi Sinai, Misri

Baraza la Usalama lalaani shambulizi Sinai, Misri

Wanachama wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wamelaani vikali mashambulizi ya kigaidi ya tarehe 29 Januari Kaskazini mwa Sinai, nchini Misri ambapo raia kadhaa waliuawa na wengine kujeruhiwa.

 Wanachama wa Baraza la Usalama wamepeleka salamu zao za rambirambi kwa familia za wahanga, serikali na watu wa Misri pamoja na kuwapa pole wale waliojeruhiwa katika mashambulizi hayo waliyoyataja kama ya kikatili.

Katika taarifa, wanachama wa Baraza la Usalama wamekariri kwamba ugaidi ni mojawapo ya tishio hatari kwa amani na usalama wa kimataifa, na kwamba matendo yoyote ya ugaidi ni makosa ya jinai na hayawezi kukubaliwa bila kujali kichechezi, mahala na wakati wowote na mtu yeyote anayeitekeleza.

Aidha, wanachama wa Baraza la Usalama wamekariri uamuzi wao wa kupambana na aina yoyote ya ugaidi, kwa mujibu wa wajibu wao chini ya Katiba ya Umoja wa Mataifa.