Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Jamii bado zina hofu potofu juu ya Ebola- IFRC

Jamii bado zina hofu potofu juu ya Ebola- IFRC

Wakati idadi ya maambukizi mapya ya Ebola ikipungua sana katika nchi za Guinea, Sierra Leone na Liberia, bado jamii zinaogopa wafanyakazi wa kibinadamu, kwa mujibu wa Muungano wa Mashirika ya Msalaba mwekendu, IFRC.

Msemaji wa IFRC Birte Haid amesema kuna hatari ya kuona ugonjwa huo usiondolewe kabisa katika baadhi ya maeneo, kwa sababu jamii zinakataa wauguzi wafikie wagonjwa.

“ Katika maeneo kama Sierra Leone na hususan Guinea, mlipuko wa Ebola umeanza upya katika baadhi ya wilaya mpya. Bado kuna maeneo ambapo ukosefu wa usalama umezidi kiasi kwamba hatuwezi kutuma timu zetu”

Msemaji huyo ameongeza kwamba huko Guinea jamii bado zinafikiria kwamba wauguzi ndio wanasambaza kirusi cha Ebola wakipulizia dawa la kusafisha.

Kwa upande wake shirika la Afya duniani WHO limethibitisha uhasama wa jamii likisisitiza umuhimu wa kufuatilia waliokuwa karibu na wagonjwa.