Operesheni dhidi ya FDLR yaongozwa na FARDC ikisaidiwa na MONUSCO

30 Januari 2015

Operesheni ya kijeshi dhidi ya kundi la waasi wa FDLR iliyoanza alhamis inaongozwa na jeshi la kitaifa la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, FARDC, likisaidiwa na Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini humo, MONUSCO.

Msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric amesema hayo alipozungumza na waandishi wa habari Ijumaa hii huku akieleza kwamba Umoja wa Mataifa unakaribisha taarifa iliyotangazwa na mkuu wa jeshi la FARDC, Didier Etumba, tarehe 29 Januari, ya kuanzishwa rasmi kwa operesheni dhidi ya FDLR.

“ Siyo operesheni ya pamoja, ni operesheni inayoongozwa na FARDC na usaidizi wa MONUSCO, na MONUSCO pamoja na FARDC watafanya tathmini ya pamoja kuhusu operesheni hizo. Ni mwelekeo unaotia moyo, ambao unaenda sambamba na maamuzi ya serikali ya DRC, Baraza la Usalama na wadau wa kikanda ya kuchukua hatua ya kijeshi dhidi ya FDLR, iwapo wangeshindwa kujisalimisha kufikia tarehe 2, Januari”

Msemaji wa Umoja wa Mataifa ameongeza kwamba serikali ya DRC ina wajibu wa kwanza katika maswala ya usalama nchini humo, ikiwa na haki ya kuanzisha operesheni dhidi ya makundi yanayotishia usalama wa raia wake.

Aidha MONUSCO, leo kupitia mtandao wa kijamii wa twitter, imeeleza kwamba mashirika ya kibinadamu yameanza maandalizi ya usaidizi wa kibindamu iwapo mapigano yatasabibisha raia kukimbia makwao

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud