Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nchi za Asia na Pasifiki zaahidi kutokomeza Ukimwi ifikapo mwaka 2030

Nchi za Asia na Pasifiki zaahidi kutokomeza Ukimwi ifikapo mwaka 2030

Nchi zipatazo 30 kutoka eneo la Asia na Pasifiki zimeahidi kuongeza kasi ya kubadili hali na kutokomeza ugonjwa wa Ukimwi katika eneo hilo ifikapo mwaka 2030. Ahadi hizo zimetolewa wakati wa mkutano baina ya serikali za Asia na Pasifiki kuhusu Ukimwi, ambao umefanyika wiki hii.

Takriban watu milioni 6 wanaishi na virusi vya HIV katika eneo la Asia na Pasifiki, na ni asilimia 33 yao tu ndio wanaopokea matibabu, aghalabu kutokana na vizuizi vya kisheria na kisera kwa upatikanaji wa huduma za HIV.

Mkakati mpya wa ushirikiano wa kikanda kwa ajili ya kutokomeza Ukimwi ifikapo mwaka 2030, unalenga kuongeza kasi ya mapambano dhidi ya HIV kwa kwa hatua mahsusi. Mkakati huo unajumuisha mpango wa ufadhili endelevu wa juhudi za kukabiliana na Ukimwi na kuhakikisha upatikanaji wa dawa za kuokoa maisha pamoja na upimaji.