Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Njaa inaathiri wakimbizi wa Nigeria nchini Cameroun- WFP

Njaa inaathiri wakimbizi wa Nigeria nchini Cameroun- WFP

Katika kipindi cha wiki chache zilizopita, idadi ya watu wanaokimbia makwao Nigeria kutafuta hifadhi nchini Cameroun imeongezeka, kwa mujibu wa Shirika la Mpango wa Chakula Duniani, WFP.

Elisabeth Byrs msemaji wa WFP mjini Geneva amesema vijiji vizima vimeteketezwa moto na waasi wa Boko Haram katika maeneo ya kaskazini mwa Nigeria, inakopakana na Cameroun, wakulima wakishindwa kwenda kulima.  Ameongeza kwamba WFP inapanga kusaidia zaidi ya watu 96,000 nchini Cameroun.

Miongoni mwao ni wakimbizi wa Nigeria, wakimbizi wa ndani katika eneo hilo la Cameroun, na watu wanaoishi katika maeneo hayo ambao wameathirika na hali hiyo na wanaokumbwa na mashambulizi na ukosefu wa usalama mpakani”  

Byrs ameeleza pia kwamba watoto wadogo na wanawake wajawazito au wanaonyonyesha watoto wako kwenye hali ngumu zaidi, wakipatiwa chakula maalum kwa ajili ya mahitaji yao.

Aidha msemaji huyo amesema WFP inahitaji dola milioni 23 kwa ajili ya operesheni zake nchini Cameroun kwa mwaka 2015, lakini asilimia 65% za mahitaji ya fedha hazijapatikana.