Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kwenye AU, Ban awamulika viongozi wasiotaka kuondoka mamlakani

Kwenye AU, Ban awamulika viongozi wasiotaka kuondoka mamlakani

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, amesema leo kuwa ubadilishaji wa katiba kwa njia isiyo ya kidemokrasia pamoja na mianya ya kisheria visitumiwe na viongozi kukataa kuondoka mamlakani. Taarifa kamili na Priscilla Lecomte.

(Taarifa ya Priscilla)

Ban amesema hayo wakati akimulika suala la demokrasia na uchanguzi katika hotuba yake kwenye mkutano wa viongozi wa Muungano wa Afrika, AU mjini Addis Ababa, Ethiopia, ambao kauli mbiu yake kuu ni kuwawezesha wanawake katika hatua za kufikia Ajenda ya Afrika ya 2063.

 "Watu kote duniani wameelezea kusikitishwa na viongozi wasiotaka kung’atuka mamlakani pale muhula wao unapomalizika. Naunga  mkono hofu yao hiyo. Mabadiliko ya katiba yasiyo ya kidemokrasia na mianya ya kisheria kamwe visitumiwe kukatalia mamlakani.”

Bwana Ban amezungumzia pia masuala mengine, yakiwemo ukatili wa Boko Haram, ambao amesema unatishia amani na usalama kitaifa, kikanda na hata kimataifa.

Kuhusu Ebola, Ban amesema juhudi zilizotumiwa katika kutokomeza polio na kupambana na Ukimwi zinadhihirisha kwamba ushirikiano unaweza kuleta ufanisi.