Operesheni ya kijeshi dhidi ya FDLR yaanza DRC

29 Januari 2015

Operesheni ya kijeshi dhidi ya waasi wa FDLR imeanza leo Alhamis, kwa mujibu wa mkuu wa jeshi la serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, DRC. Taarifa zaidi na Abdullahi Boru.

(Taarifa ya Abdullahi)

Alipozungumza na waandishi wa habari mjini Beni, Kivu Kaskazini, jenerali Didier Etumba, mkuu wa FARDC, amesema operesheni hii iitwayo « Sokola2 » inatekelezwa kwa ushirikiano na ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini humo, MONUSCO.

Jenerali huyo ameongeza kwamba idadi ya FDLR imepungua na kwa sasa hawazidi wajeshi 1,400.

Kwa upande wake, mkuu wa MONUSCO, Martin Kobler, alipozungumza na waandishi wa habari Jumatano, amesema muda umefika kuanza operesheni za kijeshi.

"Tunapaswa kutwaa vijiji na maeneo wanayotawala. Kwa hiyo tunapswa kuanza kwa sababu hata kama itachukua muda, tunapaswa kuanza sasa hivi… kwa sababu kila mtu amechoka kusubiri. Baraza la Usalama limechoka kusubiri, raia wamechoka kusubiri hapa. Haiwezekani tena kukaa na FDLR. Utaratibu wa kujisalimisha kwa amani umeshindwa, sasa ni wakati wa kuanza operesheni kwa ukweli " 

Kobler ambaye amewasili katika mkutano wa Muungano wa Afrika nchini Ethiopia alhamis hii anatakiwa kujadili na viongozi wa Afrika kuhusu utaratibu huo.

Wakati huo huo, Baraza la Usalama limepitisha azimio la kuongeza muda wa vikwazo vya silaha DRC hadi tarehe mosi Julai mwaka 2016, na kulaani makundi yaliyojihami mashariki mwa DRC.

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter