29 Januari 2015
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni, UNESCO, Irina Bokova, ameelezea kusikitishwa mno na mauaji ya mtangazaji wa televisheni, Ali Al-Ansari kwenye kata ya Diyala, kaskazini mashariki mwa Baghdad mnamo Januari tarehe 23.
Mwanahabari huyo anayefanya kazi na kituo cha televisheni cha Al-Ghadeer, aliuawa wakati akiripoti kuhusu operesheni ya vikosi vya usalama Iraq dhidi ya makundi yenye msimamo mkali.
Bi Bokova amelaani mauaji hayo, akisema kuwa anasikitishwa sana na kuuawa kwa wanahabari wengi wanaoripoti kuhusu mzozo nchini humo.
Ameongeza kuwa idadi kubwa ya vifo vya wanahabari inatatiza uwezo wa vyombo vya habari kutoa habari muhimu kwa umma.