Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNESCO yalaani mauaji ya wanahabari 5 Sudan Kusini

UNESCO yalaani mauaji ya wanahabari 5 Sudan Kusini

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni, Irina Bokova, amelaani mauaji ya wanahabari watano nchini Sudan Kusini, na kutaka hatua zichukuliwe kuimarisha usalama wa wanahabari nchini humo.

Bi Bokova amelaani mauaji ya Musa Mohammed Dahiyah, Butrus Martin Khamis, Dalia Marko, Randa George Adam, na Adam Juma Adam, akisema vifo vyao ni pigo kubwa kwa uhuru wa habari na kujieleza.

Ametoa wito kwa mamlaka za Sudan Kusini kufanya kila liwezekanalo kuhakikisha kuwa uhuru huo unalindwa, na pia kwamba wanahabari wanaweza kutimiza majukumu yao katika mazingira salama.

Wanahabari hao watano waliuawa mnamo Januari tarehe 25 na watu waliojihami wasiojulikana, wakati walipokuwa wakisafiri kwenye msafara na viongozi wa mikoani katika jimbo la Bahr el Ghazal Magharibi.