Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Dola bilioni 3.1 zahitajika kuwasaidia watoto milioni 62- UNICEF

Dola bilioni 3.1 zahitajika kuwasaidia watoto milioni 62- UNICEF

Shirika la Kuhudumia Watoto katika Umoja wa Mataifa, UNICEF, limesema kuwa migogoro inayozidi kuwa sugu na haribifu imefanya kazi yake kuwa ngumu zaidi, wakati likitoa ombi la dola bilioni 3.1. Taarifa zaidi na Joshua Mmali.

(Taarifa ya Joshua)

UNICEF inapanga kutumia fedha hizo kuwasaidia watu katika nchi zilizoathiriwa moja kwa moja na mapigano kama vile Syria, lakini pia zile ambazo hazimulikwi sana na vyombo vya habari, kama vile Sudan Kusini.

Halikadhalika, shirika hilo limesema kuwa ufadhili unahitajika Liberia, Guinea na Sierra Leone siyo tu kwa kutokomeza Ebola, lakini pia kukarabati mifumo ya afya ya msingi katika nchi hizo zilizoathiriwa zaidi na mlipuko wa Ebola.

Afshan Khan, ni Mkurugenzi wa Mipango ya Dharura katika UNICEF.

“Watoto zaidi wameathiriwa. Ukizingatia Syria, wakimbizi wanaingia Lebanon na kuweka shinikizo kubwa kwa huduma haba zinazopatikana katika maeneo yenye umaskini zaidi.”

Fedha zilizoombwa, ambazo ni dola bilioni 1 zaidi ya zile zilizoombwa mwaka uliopita, zitatumiwa kuwasaidia watoto wapatao milioni 62 katika nchi 71, kiasi kikubwa zaidi kikienda Syria na maeneo mengine yenye migogoro kama vile Nigeria.