Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Safari ya kujenga kustahimiliana bado ni ndefu: Ban

Safari ya kujenga kustahimiliana bado ni ndefu: Ban

Ghasia na upendeleo unaodhihirika kila siku vinakumbusha dunia kuwa safari ya kusimamia haki, kuepusha mauaji ya kimbari na kutetea utu wa binadamu bado ni ndefu. Ni ujumbe wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon aliotoa leo ikiwa ni miaka 70 tangu majeshi ya washirika yakomboea kambi ya mateso ya Auschwitz Birkenau, ambayo utawala wa manazi wa Ujerumani uliitumia dhidi ya mayahudi. Taarifa zaidi na Assumpta Massoi.

(Taarifa ya Assumpta)

Akitoa ujumbe wake Ban  amesema kumbukizi ya leo inafanyika huku dunia ikikubwa na majaribu makubwa kwa misingi ya yale yaliyotokea huko Ujerumani.

Amesema manazi waliuwa mamilioni ya watu wengi wao wakiwa wayahudi kwa misingi ya rangi na kwamba walikuwa wachache na zama za sasa makundi madogo bado yanakumbwa na ubaguzi.

Amesema mivutano ya kidini inaendelea na jamii zilizo hatarini zinazidi kuzika ndugu zao huku zikiishi kwa hofu bila kusahau chuki dhidi ya wayahudi.

Ban amesema Umoja wa Mataifa uliundwa baada ya janga la vita vikuu vya pili vya dunia na mauaji ya Holocause, hivyo azma yake ni kuendelea kulinda makundi yaliyo hatarini, kutetea haki za binadamu na kusimamia uhuru, utu na hadhi ya binadamu.

Hivyo ametaka jamii ya kimataifa kusimama kidete kung’oa mizizi ya chuki na ile ya kutostahimiliana.