Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kamishna Zeid awakumbuka wahanga wa Holocaust

Kamishna Zeid awakumbuka wahanga wa Holocaust

Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu Zeid Ra’ad Al Hussein, ametoa wito kwa kila mtu aimarishe ujasiri wake kimaadili, ili kuwaenzi wahanga na manusura wa mauaji ya halaiki ya Holocaust. Taarifa kamili na Grace Kaneiya.

(Taarifa ya Grace)

Kamishna Zeid amesema hayo wakati ulimwengu unapoadhimisha miaka 70 tangu kukombolewa kwa kambi ya Auschwitz-Birkenau- moja ya kambi ambako yalitekelezwa mauaji ya Holocaust, yaliyopangwa na serikali ya Nazi.

Kamishna Zeid amesema mamilioni ya watu waliuawa kwa ajili ya ubaguzi, lakini bado kuna chuki za kibaguzi kwa misingi ya rangi na kabila, huku mauaji yanayochochewa na chuki hizi yakiendelea. Amesema ubaguzi na chuki huua na kujeruhi maelfu ya watu, na pia kumdhuru kila mmoja mtu.

Kamishna Zeid amekumbusha kuhusu Katiba ya Umoja wa Maataifa, ambayo pia inaadhimisha miaka 70 mwaka huu tangu ipitishwe, akisema ili kutimiza ndoto za katiba hiyo, kila mmoja anapaswa kupinga aina zote za ubaguzi, ili kuishi kwa uhuru, heshima, usawa na haki.