Mchakato wa mazungumzo kuhusu Darfur wazinduliwa El Fasher.
Ujumbe wa pamoja wa Umoja wa Mataifa na Muungano wa Afrika huko Darfur, UNAMID umezindua mchakato wa Mazungumzo na Mashauriano ya ndani ya Darfur, DIDC katika Chuo Kikuu cha El Fasher, Kaskazini mwa Darfur hivi leo.
Tukio hilo liliwaleta pamoja viongozi wa Serikali ya Sudan na Maafisa wa Mamlaka ya jimbo la Darfur, DRA , wanachama wa Kamati ya Utekelezaji wa DIDC, wawakilishi wa asasi za kiraia Darfur, wakimbizi wa ndani na maafisa wa UNAMID.
Wakati wa uzinduzi wa mchakato huo, wasemaji walisisitiza umuhimu wa DIDC kama hatua stahiki katika utekelezaji wa makubaliano ya Doha kwa ajili ya amani ya Darfur, DDPD na jitihada za kuleta amani na utulivu katika mkoa huo.
Naibu Mwakilishi Maalum wa Pamoja wa UNAMID, Abdul Kamara ameelezea umuhimu wa DIDC huku akikariri kujitolea kwa UNAMID katika utekelezaki wake.
Halikadhalika, Bw Kamara amesema DIDC itatoa fursa ya kuimarisha amani, kukuza na kujenga imani pamoja na kuhimiza maridhiano na umoja miongoni mwa watu wa Darfur na Sudan kwa ujumla.