Kuna nuru sasa ya matumizi ya nishati ya nyuklia:IAEA

26 Januari 2015

Mkurugenzi Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la nishati ya atomiki, IAEA Yukia Amano amesema dunia hivi sasa inashuhudia kuibuka upya kwa nishati ya nyuklia.

Akizungumza huko Singapore Jumatatu, Yukia amesema hilo linatokana na kuongezeka kwa idadi ya nchi zinazofikiria kujenga mitambo ya nyuklia ili kukidhi ongezeko la mahitaji ya kiuchumi huku zikipunguza utoaji wa gesi chafuzi.

Ametaja manufaa ya nishati ya nyuklia ikiwemo kuimarisha uhakika wa upatikanaji wa nishati, kupunguza athari za ongezeko la mafuta yatokanayo na kisukuku na hata mabadiliko ya tabianchi.

Mkuu huyo wa IAEA amesema miaka mitano tangu janga la mtambo wa nyuklia wa Fukushika, hatua za kiusalama zimechukuliwa ikiwemo tafiti ya kuwa na mitambo ya kisasa inayoweza kuwa salama zaidi.

Amesema kuna fursa kubwa kwa mataifa madogo kushirikiana kikanda ili kuwa na miradi ya nishati ya nyuklia akisisitiza kuwa IAEA haina ushawishi wowote kwa nchi kuamua kutumia au kutotumia nishati hiyo.

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter