Tuko pamoja na wananchi wa Haiti kuhusu uchaguzi:Baraza

26 Januari 2015

Wajumbe wa Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa ambao wametembelea Haiti ili kuonyesha mshikamano na nchi hiyo wamesema wako tayari kutoa usaidizi kuhakikisha uchaguzi wa mwaka huu wa 2015 unafanyika kama ulivyopangwa.

Hiyo ni kwa mujibu wa Mwakilishi wa Kudumu wa Marekani kwenye Umoja wa Mataifa Balozi Samantha Power ambaye ni mmoja wa wajumbe wa baraza hilo walioko kwenye ziara hiyo ya siku tatu.

Ziara yao imefanyika wakati huu nchi hiyo iko kwenye mzozo wa kisiasa kutokana na kutofikiwa makubaliano ya kufanyika kwa chaguzi za ngazi ya manispaa na bunge.

Balozi Power amesema Umoja wa Mataifa umekuwa kidete na Haiti wakati wa shida na raha.

(Sauti ya Balozi Power)

Mkataba wa demokrasia kati ya watawala na watawaliwa ni sehemu muhimu sana kwa maendeleo ya Haiti na sisi Baraza la Usalama tunataka kutoa usaidizi wetu wote tunaoweza ili kuhakikisha chaguzi zinafanyika kama ilivyopangwa 2015 na kuhakikisha wananchi wote wa Haiti wanawekeza kwenye demokrasia, uchumi na maendeleo ya nchi hii.”

Balozi Cristián Barros Melet wa  Chile, ambaye ni kiongozi mwenza wa ujumbe huo wa baraza la usalama kwenye ziara hiyo amesema mazungumzo yao na Rais Michel Martelly yalikuwa ya kuvutia ambapo walitumia pia fursa hiyo kubadilishana mawazo kuhusu hali inayoendelea nchini Haiti.

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter