Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WFP yaongeza juhudi zake za misaada Malawi japo kuna changamoto za fedha

WFP yaongeza juhudi zake za misaada Malawi japo kuna changamoto za fedha

Shirika la Mpango wa Chakula Duniani, WFP limeanza usambazaji wa biskuti zenye virutubisho vya juu zaidi kwa wahanga wa mafuriko wilayani Nsanje, mojawapo ya maeneo yaliyoathiriwa kwa kiasi kikubwa na mafuriko Kusini mwa Malawi.

Msaada huo wa tani 77 unaoweza kuwalisha watu 77,000 ulipelekwa kwa ndege hadi nchini Malawi kutoka ghala ya Umoja Mataifa lililoko Dubai mapema wiki hii.

WFP limesema walengwa ni watu wanaoishi katika mazingira magumu, hasa watoto, ambao wamelazimika kukimbia makazi yao kutokana na mafuriko.

Kwa mujibu wa WFP kufikia maeneo yaliyoathirika zaidi na kutathmini mahitaji imekuwa vigumu sana kwani barabara nyingi na madaraja yameharibiwa au kusombwa na maji.

Kulingana na takwimu za hivi karibuni kutoka kitengo cha Usalama wa chakula nchini, baadhi ya watu 370,000 wanahitaji chakula haraka pamoja na misaada mengine.