Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza la Usalama laanza ziara Haiti

Baraza la Usalama laanza ziara Haiti

Wanachama wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wanaanza leo ziara ya siku tatu nchini Haiti, wakitarajia kutua Port-au-Prince na Cap-Haïtien. Ziara hiyo itaongozwa na mwakilishi wa kudumu wa Chile, ambaye ni rais wa Baraza hilo kwa mwezi huu wa Januari, na mwakilishi wa kudumu wa Marekani.

Baraza la Usalama linatazamia kuitumia ziara hiyo kama hakikisho la uungaji mkono wake endelevu kwa serikali ya Haiti na watu wake. Baraza hilo pia litaitumia ziara hiyo kuwahimiza wadau wa kisiasa wa Haiti kushirikiana katika kuhakikisha kuwa uchaguzi wa maseneta na serikali za mitaa unafanyika bila kuchelewa, kwa njia huru, jumuishi, haki na uwazi.

Halikadhalika, wanachama wa Baraza la Usalama watafanya tathmini ya utekelezaji wa maazimio ya Baraza hilo kuihusu Haiti, likiwemo 2180, na jinsi taifa hilo linavyoendelea kukuza uwezo wake katika kuimarisha polisi, na uwezo wa mamlaka za kitaifa kutimiza wajibu wa kuweka usalama na utulivu nchini.

Wakati wa ziara hiyo, wanachama wa Baraza la Usalama wanatarajiwa kukutana na Rais Martelly na maafisa wengine wa ngazi ya juu serikalini, pamoja na wawakilishi wa mashirika ya kibinadamu na nchi zinazochangia vikosi vya kuweka utulivu Haiti, MINUSTAH.