DRC msitumie nguvu kupita kiasi dhidi ya waandamanaji: OHCHR

23 Januari 2015

Ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa imesema ina hofu kutokana na vitendo vya maafisa wa usalama huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC kutumia nguvu kupita kiasi dhidi ya waandamanaji wanaopinga rasimu ya sheria ya uchaguzi inayotaka kufanyika kwa sense ya watu kabla ya uchaguzi.Taarifa zaidi na Priscilla Lecomte.

(Taarifa ya Priscilla)

Maandamano hayo yaliyoanza tarehe 19 mwezi huu tayari yamesababisha vifo vya watu 13 na wengine 30 wamejeruhiwa.

Kwa sasa rasimu hiyo imeshapitishwa na bunge la chini na imewasilishwa kwa baraza la seneti ambapo Ofisi ya haki za binadamu ina wasiwasi kuwa iwapo itapitishwa inaweza kusababisha vurugu zaidi. Rupert Colville ni msemaji wa ofisi hiyo ya haki za binadamu.

(Sauti ya Rupert)

“Tunatoa wito kwa serikali ya DRC kufanya uchunguzi wa kina na huru haraka iwezekanvyo juu ya matumizi ya ziada ya nguvu hususan matumizi ya risasi dhidi ya waandamanaji.  Matumizi ya nguvu za ziada  ya aina yeyote wakati wa maandamano ni lazima yafanywe ikiwa kuna umuhimu, na yatumike sawia na kwa uangalifu iwapo ni lazima. Silaha zitumike tu wakati ambapo kuna umuhimu wa kuokoa maisha. Na tunatoa wito kwa waandamanaji kujizuia na vitendo vya uhalifu na ukorofi.”

Uchaguzi mkuu wa DRC umepangwa kufanyika mwaka 2016.

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter