Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wekeza katika kupunguza gesi ya mkaa- Ban

Wekeza katika kupunguza gesi ya mkaa- Ban

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, amesema kuwa kupunguza uzalishaji wa gesi chafuzi za mkaa ni lazima kuwe sehemu ya mipango ya uwekezaji na maendeleo katika miongo ijayo. Taarifa zaidi na Amina Hassan..

(Taarifa ya Amina)

Akizungumza kwenye jukwaa la kiuchumi duniani huko Davos, Uswisi, Ban ametoa wito kwa serikali na wafanyabiashara kufanya chaguo la busara, kwa kuchagua barabara ya uwekezaji unaozalisha gesi ya mkaa kwa kiwango cha chini, akiutaja mwaka wa 2015 kama mwaka wa kuchukua hatua duniani.

Ban amesema ripoti ya jopo la pamoja la serikali kuhusu mabadiliko ya tabianchi, IPCC, imeweka bayana kuwa mabadiliko ya tabianchi yamefanyika kwa sababu ya vitendo vya wanadamu, na kwa hiyo ni wajibu wa wanadamu kukabiliana na suala hilo, akiongeza kwamba bado inawezekana kuchukua hatua mathubuti sasa.

“Sisi ndicho kizazi cha kwanza kinachoweza kutokomeza umaskini, na kizazi cha mwisho kinachoweza kuchukua hatua kuepusha athari mbaya zaidi za mabadiliko ya tabianchi. Vizazi vijavyo vitatuhukumu iwapo tutashindwa kutimiza wajibu wetu wa kimaadili na kihistoria.”

Ban ametoa wito kwa viongozi wa dunia kuweka ahadi zitakazochochea kasi ya ushindi, akiwataka waounnyeshe ulimwengu kuwa uzalishaji mdogo wa gesi chafuzi ya mkaa siyo tu kitu stahiki kufanya, bali pia ni chaguo la busara kwa maendeleo endelevu kwa wote.