Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nimejifunza kutoka kwa shujaa wa njaa duniani: Ban

Nimejifunza kutoka kwa shujaa wa njaa duniani: Ban

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon ameelezea kuguswa kwake na mchango wa mjumbe wa amani wa Umoja huo binti mfalme Haya Al Hussein ambaye leo amepatiwa tuzo ya shujaa wa njaa duniani kwa mwaka 2015.

Akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi tuzo hiyo inayhutolewa na shirika la mpango wa chakula duniani, WFP Ban amesema binti mfalme Haya amekuwa mstari wa mbele kupiga vita njaa na utapiamlo kwenye nchi mbali mbali ikiwemo zile zilizoko barani Afrika.

Ametolea mfano tetemeko la ardhi la Haiti mwaka 2010 ambapo binti mfalme huyo alikwenda nchini humo kupeleka chakula cha msaada na maji safi na salama kwa maelfu ya wahanga na hata kukabidhi ofisi ya muda inayohamishika ya Rais.

Katibu Mkuu amesema moyo huo wa kutenda mambo ni wa kipekee akisema..

(Sauti ya Ban)

“Uliwahi kusema kuwa dunia yetu imefilisika kimaadili kwa sababu tunaweza kutumia matrilioni ya dola kununua silaha tunapopigania ardhi, itikadi na dini huku tukiachia watoto Milioni 300 wakifa kwa njaa. Nimeguswa sana na maneno yako na zaidi ya yote maarifa yako, ujasiri na azma yako ya kubadili dunia.”