Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban asikitishwa na kuzorota kwa amani DRC

Ban asikitishwa na kuzorota kwa amani DRC

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban ki-Moon ameelezea kusikitishwa kwake na kuzorota kwa amani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo DRC hususan mji mkuu Kinshasa na miji mingine kufuatia kupitishwa kwa rasimu ya sheria ya uchaguzi.

Taarifa ya msemaji wa Umoja wa Mataifa imemkariri Ban akisema anahuzunishwa pia na vifo na majeruhi na kutaka vikosi vya ulinzi nchini humo pamoja na waandamanaji kujizuia ili kuepuka machafuko zaidi .

Katibu Mkuu ameelezea umuhimu wa jukumu la serikali katika kuwezesha uhuru wa kujieleza kwa amani na pia umuhimu wa waandamanaji kufanya hivyo kwa amani. Amesema machafuko hayakubaliki sanjari na maandamano ya vurugu.

Bwan Ban ametaka wadau kurejelea mazungumzo ya amani ya kisiasa na kuhakikisha masuala ya uchaguzi yanajadiliwa kwa njia jumuishi na ya amani katika jukwaa mujarabu.

Pia ameelezea utayari wa mwakilishi maalum kutumia ofisi yake kupunguza tofauti kati ya wahusika wakuu na kusisitiza uchaguzi wa amani, na heshima kulingana na katiba.