Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mjumbe wa amani wa UM kupatiwa tuzo ya shujaa dhidi ya njaa 2015:WFP

Mjumbe wa amani wa UM kupatiwa tuzo ya shujaa dhidi ya njaa 2015:WFP

Shirika la mpango wa chakula duniani, WFP linampatia tuzo ya shujaa dhidi ya njaa kwa mwaka 2015, binti mfalme wa Jordan, Haya Al Hussein.

Sherehe ya kumkabidhi tuzo hiyo itafanyika huko Davos, Uswisi wakati wa mjadala kuhusu wanawake na ubunifu katika kongamano la uchumi la dunia.

Binti mfalme huyo wa Jordani ni mjumbe wa amani wa Umoja wa Mataifa na pia mwenyekiti wa taasisi ya kibinadamu ya kimataifa ya jiji la Dubai, ambako ni kitovu cha bohari ya vifaa vya misaada ya kibinadamu.

Anatambulika kwa jinsi alivyoshughulikia masuala ya njaa maeneo mbali mbali duniani ikiwemo nchini mwake Jordan kwa kuanzisha taasisi ya kwanza isiyo ya kiraia inayohusika na usaidizi wa chakula huko mashariki ya kati, Tikiyet Um Ali.

WFP inasema kila familia nchini Jordan ambayo haiwezi kujipatia chakula, sasa inapatiwa mgao kila mwezi na taasisi hiyo isiyo ya kiserikali imekuwa na dhima muhimu katika kulisha familia wakati wa mzozo wa Gaza mwaka jana.