Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ufadhili wa umma kwenye elimu unalenga watoto wa matajiri: Ripoti

Ufadhili wa umma kwenye elimu unalenga watoto wa matajiri: Ripoti

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF limesema ni kiwango kidogo sana cha rasilimali za umma kinatumika kuelimisha watoto maskini kwenye nchi zinazoendelea ikilinganishwa na nchi tajiri.

Ripoti hiyo iitwayo uwekezaji kwa ajili ya elimu na uwiano, imetolewa huko Davos wakati wa kongamano la uchumi la dunia ikisema kuwa tofauti hiyo ni mara 18 ikisema katika nchi hizo maskini mara nyingi wanufaika wa usaidizi wa elimu ni watoto wanaotoka familia zenye uwezo na husomeshwa hadi elimu ya  juu.

Naibu Mkurugenzi  Mtendaji wa UNICEF, Yoka Brandt amesema hiyo si sahihi kwani hali hiyo huacha watoto wa familia za vipato vya chini wakipata elimu isiyo bora kutokana na sababu mbali mbali ikiwemo umaskini, ulemavu, na mizozo.

Kwa mantiki hiyo ripoti inataka serikali na wahisani kupatia kipaumbele mahitaji ya watoto hao wa kaya maskinmi kwani elimu ni jawabu la kumaliza umaskini uliodumu kwa watoto hao na familia  zao.

Ripoti inasema asilimia Tano tu ya faida ya mwaka ya kampuni 15 zenye mapato makubwa zaidi duniani, inaweza kumaliza pengo la dola bilioni 26 kwa mwaka zinazotakiwa ili kutimiza lengo la elimu kwa wote kwenye nchi 46 za vipato vya chini duniani.