Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kamishna mkuu wa haki za binadamu alaani kutukanwa kwa mtaalam maalum Myanmar

Kamishna mkuu wa haki za binadamu alaani kutukanwa kwa mtaalam maalum Myanmar

Kamishna mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa Zeid Ra’ad Al Hussein amesema jumatano hii kwamba dhihaka dhidi ya Mtalaam maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki za binadamu nchini Myanmar, Yanghee Lee, haikubaliki.

Katika taarifa iliyotolewa jumatano hii, Kamishna Zeid amesema lugha ya kashfa iliyotumiwa na kasisi mmoja maarufu dhidi ya Bi Yanghee Lee haistahimiliki, na amewaomba viongozi wa kidini na kisiasa Myanmar kulaani hadharani aina zote za chuki na hasa mashambulizi binafsi dhidi ya Mtaalam wa Umoja wa Mataifa.

Badala la kumshambulia Bi Lee, Kamishna Zeid amewaomba viongozi hao pamoja na jamii kushughulikia hoja zilizoibuliwa na mtalaam huyo.  

Bi Lee, kwa mujibu wa mkataba wake, alikwenda Myanmar ili kutathmini hali ya watu wa jamii ya Rohingya na maswala ya haki za binadamu nchini humo.

Licha ya kupongeza juhudi za viongozi wa dini ili kuendeleza mshikamano wa jamii, ameeleza wasiwasi wake juu ya wakimbizi wa ndani wenye asili ya Rohingya, ambao wanaishi kwenye mazingira magumu.

Aidha ametoa onyo dhidi ya mradi za sheria mpya inayoweza kuzidisha ubaguzi dhidi ya makundi madogo ya kidini na kikabila.