Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hali ni mbaya Ukraine, majadiliano ndiyo njia pekee ya utatuzi : Feltman

Hali ni mbaya Ukraine, majadiliano ndiyo njia pekee ya utatuzi : Feltman

Licha ya kuendelea kwa machafuko nchini Ukraine diplomasia ni njia pekee ya kusuluhisha mgogoro wa Ukraine amesemaMkuu wa Masuala ya Kisiasa katika Umoja wa Mataifa, Jeffrey Feltman akilihituhubia baraza la usalama la Umoja wa Mataifa katika kikao kilichojadili hali nchini humo.

Bwana Feltman amesema licha ya makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyofikiwa mwezi September mwaka jana bado mapigano yanaendelea na kwamba hali hiyo haivumiliki.

(SAUTI FELTMAN)

"Kama Katibu Mkuu alivyorudia na kusisitiza , hakuna njia mbadala ya moja kwa moja zaidi ya majadiliano ya ujenzi wa amani . Utekelezaji wa usitishwaji wa mapigano ambao kwa sasa ni jina tu, unahitajika kwa dharura kwa pande zote na ni jambo la msingi"

Mkuu huyo wa Masuala ya Kisiasa katika Umoja wa Mataifa amesema inasikitisha kuona kuwa nchi ambayo mwaka mmoja uliopita ilikuwa haina watu ambao hawana makazi sasa inashuhudia zaidi ya watu laki nane wakiwa wamepoteza makazi ndani ya nchi na zaidi ya laki sita wakiwa wakimbizi nje ya nchi.

Kwa upande wao wawakilishi wa Lithuania, Marekani na Urusi wametaka kukomeshwa kwa mapigano mara moja kwa kuheshimu makubaliano ya kuweka silaha chini kwa pande zote.