Hafla yafanyika UM kadhimisha miaka 70 tangu kuokolewa kwa kambi ya Auschwitz-Birkenau

21 Januari 2015

Hafla maalum imefanyika leo kwenye Umoja wa Mataifa kuadhimisha miaka 70 tangu kukombolewa kwa kambi ya Auschwitz-Birkenau, ambayo ilitumiwa na serikali ya Ujerumani ya Nazi kutekeleza mauaji ya kimbari.

Kauli mbiu ya hafla hiyo ambayo imeandaliwa na Ubalozi wa Kudumu wa Poland kwenye Umoja wa Mataifa ni swali: “Kwa nini tumeshindwa kuzuia mauaji ya kimbari, na ni vipi tunaweza kubadili hali hii?”

Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Mwakilishi wa Kudumu wa Polanda Boguslaw Winid amesema

“Watu milioni 1.1 walipoteza maisha yao kwenye kambi ya ki-Nazi ya Ujerumani, ya maangamizi Auschwitz-Birkenau. Asilimia 90 kati yao walikuwa Wayahudi. Wahanga wengine walikuwa raia wa Polanda, Urusi, Belarus, Ukraine, Waroma na wengine kutoka nchi za Ulaya. Leo tunakumbuka uhalifu huo kwa matumaini kuwa siku moja, ulimwengu hautakuwa tena na mauaji ya kimbari na kikabila.”

Naye Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Jan Eliason, amesema leo ni siku ya kutafakari

“Leo, tutafakari, mabibi na mabwana, waheshimiwa na marafiki, kuhusu njia bora ya kuzuia na kulinda ulimwengu wetu kuwa tena jukwaa la uhalifu kama ulioshuhudiwa wakati wa Holocaust, kwenye nyanja za mauaji Cambodia, mauaji ya kimbari Rwanda na Srebrenica. Ni muhimu tutathmini ni kwa nini tunaendelea kushindwa kuzuia mauaji ya halaiki, licha ya mafunzo tuliyopata, licha ya kufahamu vyanzo na vichochezi, na licha ya mahakikisho yetu ya kuwa, kamwe yasitokee tena.”

Amesema ni lazima kila mmoja ajiulize ni nini zaidi kinachoweza kufanyika, na kwa njia tofauti ili kuwalinda watu na kujenga jamii ambapo kuvumiliana kunashinda chuki..

“Mauaji ya kimbari yanaweza tu kufanyika iwapo tunapuuza dalili za kuonya, na kutotaka kuchukua hatua.”

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter