Asia: adhabu za kifo kwa msingi wa biashara ya madawa ya kulevya zatiwa wasiwasi

20 Januari 2015

Ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa imeeleza wasiwasi wake kuhusu matumizi ya adhabu ya kifo dhidi ya uhalifu unaohusiana na biashara ya madawa ya kulevya katika Ukanda wa Kusini Mashariki mwa Asia. Akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva, Ravina Shamdasani ambaye ni msemaji wa Ofisi hiyo amesema kwamba watu sita waliohukumiwa adhabu ya kifo nchini Indonesia tayari wameuawa siku ya jumapili, huku wengine 60 wakisubiri kutekelezwa kwa adhabu yao kwa kujihusisha na biashara ya madawa ya kulevya. Amesisitiza wasiwasi wa ofisi yake baada ya Rais wa Indonesia kuazimia kwamba maombi ya msamaha hayatasikilizwa. “ Kwa mujibu wa mkataba wa kimataifa juu ya Haki za Raia na kisiasa, ambao umeridhiwa na Indonesia, kila mtu anayehukumiwa adhabu ya kifo anapaswa kuwa na haki ya kuomba msamaha au adhabu yake ibadilishwe. Tunaziomba mamlaka za Indonesia kusitisha adhabu ya kifo, na kuendesha tathmini juu ya maombi yote ya msamaha ili adhabu zibadilishwe” Aidha, nchini Vietnam, watu wanane wakiwemo wanawake wawili wameripotiwa kuhukumiwa kifo kwa msingi wa biashara ya dawa za kulevya aina ya heroin, Ofisi ya Haki za Binadamu ikiiomba Vietnam isitishe adhabu hizo. Katika Ukanda wa Kusini Mashariki mwa Asia, biashara za madawa ya kulevya ni uhalifu unaoweza kuhukumiwa adhabu ya kifo, Ofisi ya Haki za Binadamu ikikumbusha kwamba, kutokana na mfumo wa sheria ya kimataifa ya haki za binadamu, uhalifu utokanao na biashara ya madawa ya kulevya, uchumi, siasa, au ngono ya jinsia moja haupaswi kuhukumiwa adhabu ya kifo.

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter