Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kamanda wa LRA aliyekamatwa aelekea The Hague

Kamanda wa LRA aliyekamatwa aelekea The Hague

Kamanda wa kikundi cha waasi cha Lord’s Resistance Army, LRA Dominic Ongwen yuko njiani akisindikizwa kwenda mahakama ya kimataifa ya uhalifu, ICC huko The Hague,Uholanzi.

Ongwen alikamatwa hivi karibuni huko Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR kufuata hati ya kumkamata iliyotolewa na mahakama hiyo tareje 8 Julai mwaka 2005.

Kiongozi huyo wa waasi anakabiliwa na mashtaka matano ikiwemo moja la uhalifu dhidi ya binadamu na manne ya uhalifu wa kivita anayodaiwa kuyatenda mwaka 2004 nchini Uganda.

Msajili wa ICC Herman von Hebel ameshukuru Umoja wa Mataifa hususan ujumbe wake huko CAR,  MINUSCA kwa ushirikiano wao katika kuwezesha kukamatwa kwa muasi huyo na kusafirishwa kwake kwenda The Hague.

Mara baada ya kufika The Hague, Ongwen atachunguzwa afya na kukutanishwa na majaji akiwa na wakili wake na hatimaye tarehe ya kufikishwa mahakamani itatangazwa.