Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mahakama ya Shari'ah ya ISIL yatekeleza uhalifu dhidi ya ubinadamu nchini Iraq- UM

Mahakama ya Shari'ah ya ISIL yatekeleza uhalifu dhidi ya ubinadamu nchini Iraq- UM

Nchini Iraq, kundi la kigaidi linalotaka kuweka dola la kiislamu lenye msimamo mkali, ISIL, limeanzisha mahakama ya kidini, yaitwayo mahakama ya Shari’ah ambayo yanatoa adhabu dhalimu kwa wanaume, wanawake na watoto.

Kwa mujibu wa Ravina Shamdasani, msemaji wa Ofisi ya Haki za binadamu, ISIL imetoa picha za adhabu hizo kwenye mtandao wa intaneti, zikiwemo picha ya mwanamke aliyerujumiwa, na ile ya wanaume wawili waliorushwa kutoka juu ya jengo baada ya kuhukumiwa kifo kwa msingi wa  ushoga, mjini Mosul. Shamdasani amesema hii ni mifano ya ISIL kutojali maisha ya binadamu katika baadhi ya maeneo ya Iraq yaliyo chini ya utawala wake.

Alipozungumza na waandishi wa habari mjini Geneva, Ravina Shamdasani ameeleza kwamba wamepokea ripoti nyingi kuhusu adhabu ya kifo dhidi ya wanawake. Adhabu hizo zinatekelezwa papo hapo baada ya hukumu ya kifo kutolewa.

“ Wanawake wenye elimu ya juu, wenye kazi nzuri, hasa wale ambao wamegombea nafasi katika uchaguzi uliopita wako hatarini. Katika wiki za kwanza za mwaka huu tu, ripoti zinaonyesha kwamba wanawake wanasheria watatu wameuawa baada ya kukatiwa adhabu ya kifo”

Msemaji wa Ofisi ya Haki za Binadamu ameongeza kwamba ISIL inahukumu na kuua raia ambao wanashutumiwa kuiunga mkono serikali ya Iraq.

Aidha ameongeza kwamba ofisi ya haki za binadamu itaendelea kufuatilia kesi za uhalifu dhidi ya haki za binadamu na uhalifu mwingine unaotekelezwa nchini Iraq, ikitarajiwa kupeleka ripoti mbele ya Baraza la Haki za Binadamu mwezi Machi.