Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kasi dhidi ya Ebola na ukwamuaji uendelee: Ban

Kasi dhidi ya Ebola na ukwamuaji uendelee: Ban

Jitihada zetu za pamoja zimewezesha kupunguza kasi ya kuenea kwa Ebola kwenye nchi tatu zilizokumbwa zaidi na ugonjwa huo, amesema Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Sam Kutesa wakati akifungua kikao cha baraza hilo kuhusu janga lililotokana na mlipuko wa ugonjwa huo.

Amesema kuna matumaini huko Guinea, Liberia na Sierra Leone huku akisema jitihada ziimarishwe ili kumaliza kabisa mlipuko huo bila kusahau harakati za kuibua uchumi wa nchi hizo ulioporomoka.

Miongoni mwa waliozungumza ni katibu Mkuu Ban Ki-Moon ambaye pamoja na kushukuru jitihada zilizofikiwa ametoa ombi rasmi kwa jamii ya kimataifa na wadau mbali mbali..

(Sauti ya Ban)

“Endelezeni jitihada hizi. Hebu tuhakikishe kuna rasilimali za kutosha kutokomeza ugonjwa huu na kuhakikisha nchi zinajikwamua. Hebu katika kipindi hiki muhimu tuendeleze mshikamano na wanachi na nchi zilizoathirika.

Mkuu mpya wa UNMEER, Ismael Ould Cheiikh Ahmed d ambaye ameshatembelea nchi zilizokumbwa na ugonjwa huo akahutubia kwa njia ya video kutoka Freetown,  Sierra Leone akisisitiza mwendelezo wa ushirikiano baina ya nchi, jamii na uratibu wa harakati zenyewe huku akisisitiza..

 

(Sauti ya Mohammed)

“Ni lazima tuiamrishe jitihada zetu za kuhamasisha jamii ili wamiliki harakati hizi. Jamii nyingi bado zinapinga na hata kukwamisha jitihada za kudhibiti mlipuko na wakati mwingine kuhatarisha maisha ya watoa huduma ya afya. Hatuwezi kushinda vita dhidi ya Ebola bila ushiriki wa jamii.”

 

Naye Naibu mwakilishi wa Kenya kwenye Umoja wa Mataifa Balozi Koki Muli akihutubia amesema katika kuunga mkono jitihada za usaidizi mapema mwezi huu wahudumu wa afya 170 wa Kenya wamekwenda Afrika Magharibi ikiwa ni sehemu ya ahadi ya wahudumu 319 wanaoungana kwenye kundi la Muungano wa Afrika.