ILO yatabiri ukosefu wa ajira utaongezeka miaka mitano ijayo
Ripoti mpya ya Shirika la Kazi Duniani, ILO imeonya kuwa ukosefu wa ajira na misukosuko ya kijamii itaendelea kuongezeka katika miaka mitano ijayo, hali ambayo inachangiwa na mwendo wa pole wa ukuaji wa uchumi, kupanuka mwanya wa ukosefu wa usawa kitabaka na migogoro.
Ripoti hiyo ya makadirio ya hali ya ajira na kijamii mwaka 2015 imesema, watu milioni 212 watakuwa hawana ajira ifikapo mwaka 2019, idadi ikiwa imeongezeka kutoka watu milioni 201 wasio na ajira sasa. Guy Ryder ni Mkurugenzi Mkuu wa ILO
“Katika mwaka huu 2015, tunatarajia ongezeko la ukosefu wa ajira duniani kwa kiwango cha milioni tatu. Kinachotia hofu zaidi ni kwamba kwa wastani, utabiri wetu unaonyesha kuongezeka kwa ukosefu wa ajira duniani, ukionyesha kupanda hadi milioni 212 mwaka 2019.”
Bwana Ryder amesema mwenendo huu wa ukosefu wa ajira unaathiri vijana zaidi
“Wale walio kati ya umri wa miaka 15 na 24 wamo hatarini mara tatu zaidi kukosa ajira kuliko watu wazima wenye uwezo wa kufanya kazi. Kiwango cha uhaba wa ajira kote duniani ni asilimia 13.”