Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kiongozi wa Anti-Balaka akamatwa CAR:

Kiongozi wa Anti-Balaka akamatwa CAR:

Huko Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR, ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini humo MINUSCA umemkamata kiongozi wa wanamgambo wa Anti-Balaka, Gaibona Rodrigue, anayefahamika pia kama Jenerali Andilo.

Msemaji wa Umoja wa Mataifa Farhan Haq amesema Andilo alikamatwa Jumamosi huko Bouca kwenye jimbo la Oouham kufuatia hati ya kumkamata iliyotolewa na ofisi ya mwendesha mashtaka nchini CAR.

Tayari kiongozi huyo wa wanamgambo wa Anti-Balaka amekabidhiwa mamlaka za CAR na amehamishiwa mji mkuu Bangui.

Andilo anakuwa kiongozi wa kwanza kabisa wa ngazi ya juu kukamatwa na MINUSCA mwaka huu wa 2015 chini ya mamlaka yake iliyopatiwa ya hatua za dharura wakati huu ambapo tangu kuanza kwa ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini CAR zaidi ya watu 200 wameshakamatwa.

Mwezi Disemba mwaka 2013, Anti-Balaka waliteka mji mkuu Bangui na kusababisha maelfu ya watu kuuawa huku wengine wakipoteza makazi.