Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

MONUSCO yazungumzia maandamano Kinshasa na Goma

MONUSCO yazungumzia maandamano Kinshasa na Goma

Umoja wa Mataifa kupitia ujumbe wake huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, MONUSCO umeeleza wasiwasi wake juu ya maandamano yaliyoghubikwa na ghasia huko Kinshasa na Goma ambayo yametokana na mjadala unaoendelea kwenye bunge na baraza la seneti kuhusu marekebisho ya sheria ya uchaguzi.

Hayo yameelezwa na msemaji wa Umoja wa Mataifa Farhan Haq alipozungumza na waandishi wa habari waliotaka kufahamu kauli ya Umoja huo kuhusu maandamano hayo ambapo amesema.

(Sauti ya Farhan)

“Ujumbe unasihi pande kujizuia na umeendelea kusisitiza umuhimu wa kuwepo kwa mchakato wa uchaguzi ulio wazi, utakaozingatia muda, wa amani na jumuishi kwa mujibu wa vipengele vya katiba.”

Katika hatua nyingine, ujumbe wa ngazi ya juu kutoka ofisi ya Umoja wa Mataifa nchini Mali, MINUSMA umetembelea eneo la Kidal, kaskazini mwa nchi hiyo kuonyesha mshikamano wao na wakazi wa eneo hilo kufuatia shambulio la mwisho mwa wiki lililosababisha kifo cha mlinda amani mmoja kutoka Chad.