Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hatua zichukuliwe kwa magonjwa yasiyoambukiza:WHO

Hatua zichukuliwe kwa magonjwa yasiyoambukiza:WHO

Ripoti mpya ya Shirika la Afya Duniani, WHO inasema juhudi za haraka za serikali zinahitajika ili kufikia malengo ya kimataifa ya kupunguza mzigo wa magonjwa yasiyo ya kuambukiza, NCD na kupunguza vifo vya mapema vya watu milioni 16, ambao hufariki dunia kabla ya kufikia umri wa miaka 70 kutokana na magonjwa ya moyo, kiharusi, saratani na kisukari.

Mkurugenzi mkuu wa WHO, Margaret Chan amesema wakati wa uzinduzi wa ripoti hiyo ya hali ya kimataifa kuhusu magonjwa yasiyo ya kuambukiza mwaka 2014 kuwa, Jumuiya ya kimataifa ina nafasi ya kubadilisha mwelekeo wa janga la NCD, akisema kwa kuwekeza tu dola 1 hadi 3 kwa kila mtu kila mwaka, nchi zinaweza kwa kiasi kikubwa kupunguza ugonjwa na vifo vitokanavyo na NCDs.

Bi Chan ameshauri katika mwaka 2015, kila nchi inahitaji kuweka malengo ya kitaifa na kutekeleza hatua ya gharama nafuu, kwani kama nchi hazitafanya hivyo mamilioni ya maisha yataendelea kupotea mapema mno.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, vifo vitokanavyo na NCD vinaweza kuzuilika zaidi mapema, ikitolea mfano idadi ya watu milioni 38 waliofariki mwaka wa 2012 kutokana na NCD, milioni 16 au asilimia 42 ilikuwa ni ya mapema na yangeepukika.