Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban Ki-moon alaani mashambulizi dhidi ya walinda amani Mali

Ban Ki-moon alaani mashambulizi dhidi ya walinda amani Mali

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amelaani vikali mashambulizi yaliyotokea jumamosi hii dhidi ya kambi ya Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Mali, MINUSMA, ambapo mlinda amani mmoja kutoka Chad ameuawa na wengine wanne wamejeruhiwa.

Tukio hilo linafuata mashambulizi kadhaa dhidi ya wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa katika maeneo ya Kidal na Gao, yakiwemo mashambulizi ya roketi dhidi ya kambi za MINUSMA au mashambulizi mengine dhidi ya magari kwa kutumia mabomu.

Katika taarifa iliyotolewa na msemaji wake, Katibu mkuu amesisitiza msimamo wa Umoja wa Mataifa wa kuisaidia Mali kupata amani. Ameongeza kwamba mashambulizi ya hivi karibuni yanaoyesha umuhimu wa kufikia maridhiano ya kisiasa kwa mzozo huo na kurejesha mamlaka za serikali katika kila sehemu ya Mali.

Ban ki-moon amepeleka salamu zake za rambirambi kwa familia ya mlinda amani aliyeuawa na kwa serikali na jamii ya Chad, akiwatakia nafuu waliojeruhiwa.

Halikadhalika, wanachama wa Baraza la Usalama wamelaani mashambulizi hayo wakizingatia majukumu ya MINUSMA kulingana na azimio la Baraza hilo, yaani kuisaidia serikali ya Mali kufikia utulivu wa kudumu.