Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Licha ya madhila baharini, idadi ya wahamiaji Italia 2014 yaongezeka

Licha ya madhila baharini, idadi ya wahamiaji Italia 2014 yaongezeka

Idadi ya wahamiaji na watu wanaoingia Italia kwa njia ya bahari ili kusaka hifadhi ilikuwa 170,000 mwaka 2014 ikiwa ni ongezeko mara nne zaidi ikilinganishwa na mwaka uliotangulia.Takwimu hizo zilizotolewa na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Italia zinaonyesha kwamba licha ya hali ya hatari baharini, wahamiaji wanaendelea kuvuka Bahari ya Meditrenia hata wakati wa msimu wa baridi, wakati ambapo idadi hiyo ilitarajiwa kupungua.

Mkuu ofisi ya shirika la kimataifa la uhamiaji , IOM nchini Italia, Federico Soda amesema  mwezi Disemba mwaka 2013 wahamiaji na watu wanaotafuta hifadhi ilikuwa 2, 701 ikilinganishwa na  watu 6,732  Desemba 2014.

Bwana Soda ameongeza  kwamba takwimu hizi zinaonyesha kwamba mtiririko huo wa wahamiaji na watu wanaosaka hifadhi  unaambatana na kuzorota kwa hali ya migogoro ya kibinadamu kwenye mataifa yanayopakana na Ulaya, ikiwa ni pamoja na vita nchini Syria na machafuko yanayosababishwa na migogoro ya kisiasa nchini Libya.

Aidha, Bwana Soda amesema wengi wa watu hao ni wale wanaokimbia vita, mateso na serikali za kiditekta.