Ofisi ya Haki za Binadamu yasikitishwa na ghasia Bangladesh
Ofisi ya Haki za Binadamu katika Umoja wa Mataifa imeelezea kusikitishwa na ghasia za kisiasa nchini Bangladesh, ambazo zimetokana na kushindwa kwa vyama viwili vikuu kutatua tofauti zao kwa njia ya amani. Ofisi hiyo imeelezea hofu kuwa huenda zikaongezeka ghasia hizo, ambazo tayari zimesababisha vifo, majeruhi na kutatiza shughuli za kila siku, kama ilivyoshuhudiwa katika maandalizi ya uchaguzi mnamo mwaka 2014.
Machafuko ya hivi karibuni nchini Bangladesh yalianza mnamo Januari 5, pale chama cha upinzani cha BNP kilipotoa wito kwa wafuasi wake kuanza mgomo wa kuvuruga usafiri, ili kuadhimisha mwaka mmoja tangu uchaguzi wa mwaka jana, ambao ulisusiwa na upinzani. Serikali ilipiga marufuku maandamano, na kumzuia kiongozi wa BNP kushiriki maandamano.
Ravina Shamdasani ni msemaji wa Ofisi ya Haki za Binadamu, Geneva,
“Kinachosikitisha zaidi ni mashambulizi ya kuchoma moto magari. Basi la umma lililojaa watu lilichomwa moto Jumanne, na kuawaua watu wanne akiwemo mtoto. Siku iyo hiyo, mshauri wa BNP alipigwa risasi na gari lake kuchomwa moto. Hapo jana, mtu mwingine mmoja aliuawa wakati basi lilipoteketezwa Kaliakor, yapata kilomita 50 kaskazini mwa Dhaka.”
Ofisi hiyo imetoa wito kwa vyama vyote vya kisiasa kujidhibiti na kukomesha machafuko
“Tunatoa pia wito kwa mamlaka kuhakikisha kuna uchunguzi wa haraka na wa haki katika mauaji yaliyofanyika, bila kujali iwapo yalitekelezwa na vyombo vya dola au upinzani. Serikali pia ihakikishe kuwa viongozi wa upinzani hawakamatwi kiholela, na kwamba hatua zote za kurejesha utulivu zinachukuliwa kulingana na sheria ya kimataifa ya haki za binadamu, pamoja na kuheshimu uhuru wa kufanya mikutano, kutembea na kujieleza”