Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Israel yaitaka Jamii ya kimataifa iache kuunga mkono madai ya Palestina

Israel yaitaka Jamii ya kimataifa iache kuunga mkono madai ya Palestina

Mwakilishi wa Kudumu wa Israel kwenye Umoja wa Mataifa, Balozi Ron Prosor, ameitaka jamii ya kimataifa iache mwenendo wa kusikiliza na kukubali kila madai yanayotolewa na Palestina dhidi ya Israel, ukiwemo mswada uliopendekezwa ukiweka masharti ya kuafikia mkataba wa amani.

Balozi Prosor amesema mapendekezo ya mswada huo yaliegemea upande mmoja, na kwamba hayakuzingatia matakwa ya Israel ya muda mrefu kuhusu usalama. Amesema mbali na hayo, mswada huo haukutaka ugaidi ukomeshwe, wala kutambua Israel kama taifa la Wayahudi.

Mwakilishi huyo wa Israel amesema kila nchi iliyopiga kura kuunga mkono mswada wa azimio la hilo la Palestina lenye kuegemea upande mmoja, iliwapa nguvu Wapalestina kuendelea na mwelekeo wao wa kutotaka mazungumzo, na hivyo kuweka vizuizi kwa mchakato wa amani.”

“Jamii ya kimataifa imeridhia mkakati barabara ya amani, lakini Wapalestina wanatafuta njia za mkato na mbinu za kupata wanachotaka pale ambapo hazipo, na kwa kufanya hivyo, kugeuza baraza jingine la kimataifa kuwa la kisiasa. Kwa kuchagua kwenda ICC, Wapalestina wamesisitiza ujumbe kuwa hawana haja na mazungumzo na hawataki kulegeza msimamo.”

Amesema jamii ya kimataifa inapaswa kuacha kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Palestina

“Waambie Wapalestina kuwa madai ya kurejea hayana msingi, na kuweka wazi kuwa amani inahitaji kulegeza msimamo, na kusisitiza kuwa warejee kwa mazungumzo ya moja kwa moja. Israel imejikita kwa kutafuta amani. Hamna anayeelewa umuhimu wa hilo kuliko sisi. Ni miji yetu na raia wetu ndio wanaolengwa na magaidi.”