Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Zeid aitaka Saudia kusitisha adhabu ya kichapo kwa bloga

Zeid aitaka Saudia kusitisha adhabu ya kichapo kwa bloga

Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu katika Umoja wa Mataifa,  Zeid Ra’ad Al Hussein ametoa wito kwa Ufalme wa Saudia Arabia kukomesha adhabu ya kichapo dhidi ya Raef Badawi, ambaye alichapwa mijeledi 50 Ijumaa ilyopita, na ambaye amepangiwa kuchapwa tena hapo kesho na kila Ijumaa hadi pale hukumu yake ya mijeledi 1,000 itakapohitimishwa.

Msemaji wa Katibu Mkuu, Stephane Dujarric, ameusoma ujumbe wa Kamishna Zeid kwa wanahabari mjini New York

Kamishna Mkuu amesema kichapo cha mijeledi ni aina moja ya adhabu katili na inayokiuka utu, akiongeza kuwa adhabu kama hiyo imepingwa chini ya sheria ya kimataifa ya haki za binadamu, hususan Mkataba dhidi ya Utesaji, ambao Saudia imeridhia. Mkuu huyo wa Ofisi ya Haki za Binadamu ametoa wito kwa mfalme wa Saudia kusitisha kichapo dhidi ya Bwana Badawi, na kufanyia marekebisho aina hii ya adhabu kali.”

Badawi ambaye ni bloga kwenye mitandao ya habari na mwanaharakati, alihukumiwa adhabu ya kifungo cha miaka 10 gerezani, kichapo cha mijeledi 1,000 pamoja na faini ya reyale milioni moja au dola 266,000, kwa sababu alifurahia uhuru wake na haki ya kujieleza kwa amani.