Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uhuru wa kujieleza uheshimiwe na mipaka isivukwe:Kutesa

Uhuru wa kujieleza uheshimiwe na mipaka isivukwe:Kutesa

Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Sam Kutesa ametaka jamii ya kimataifa iongeze maradufu jitihada zake katika kukabiliana na vitendo katili vya magaidi kote duniani.Akizungumza na waandishi wa habari mjini New York, Marekani kuhusu programu ya mwaka huu ya mkutano wa 69 wa Baraza analoongoza, Kutesa pamoja na kulaani mashambulizi ya hivi karibuni kuanzia kule Nigeria hadi Ufaransa huku akitetea uhuru wa kujieleza amesema…

(Sauti ya Kutesa)

“Uhuru wa kujieleza kama ulivyo uhuru wa kuabudu na uhuru wa kujieleza ni haki za msingi kwa hiyo nadhani ni haki. Sasa nini hatua za serikali na taasisi nyingine? Nadhani tunapaswa kufanya mambo mawili. Mosi, kuhakikisha haki ya uhuru wa kujieleza inalindwa kwa asilimia Mia Moja, lakini pia nadhani kuna umuhimu wa kuzingatia uwajibikaji ili tusivuke mpaka.”

Rais huyo akaulizwa na waandishi wa habari iwapo anataka jitihada tu zichukuliwe au hoja hiyo ataiwasilisha barazani.

(Sauti ya Kutesa)

“Hapana nadhani tutaliwasilisha rasmi kwenye baraza kuu kwa kuwa siyo tu Paris, ni Nigeria,ni Al Shabaab, ni Al Qaeda! Ni suala la ujumla la ugaidi na misimamo mkali. Nadhani tunapaswa kulijadili rasmi.”

Katika mkutano huo alitaja hoja zitakazopatiwa kipaumbele kuwa ni pamoja na mjadala wa ajenda endelevu baada ya mwaka 2015 na mabadiliko ya tabianchi.