Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UM kusaidia wakimbizi wa Dhuluiya nchini Iraq

UM kusaidia wakimbizi wa Dhuluiya nchini Iraq

Umoja wa Mataifa na washirika wake wanafanya kazi kwa pamoja kushughulikia mahitaji ya mamia ya familia waliofurushwa makwao kufuatia mapigano katika mji uliokombolewa wa Dhuluiya, ulioko kaskazini mwa Baghdad mji mkuu wa Iraq.

Kaimu Mratibu wa Misaada ya Kibinadamu wa Umoja wa Mataifa nchini Iraq, Neil Wright amesema wanafanyakazi kwa karibu na mamlaka ya serikali za mitaa na wadau wengine kuhakikisha kuwa wanawafikia watu walio na mahitaji.

Tayari shirika la mpango wa chakula duniani,WFP, likishirikiana na lile la kuwahudumia Watoto UNICEF, limesambaza mgao wa chakula ya siku tatu kwa familia 500 kupitia serikali za mitaa, huku Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi, UNHCR likitoa mahitaji muhimu ikiwa ni pamoja na mitungi ya maji, blanketi, na vifaa vya kujisafi.

Wakati huo huo, shirika la Muslim Aid, na Shirika la Afya Duniani, WHO zimepeleka vifaa tiba katika kituo cha afya vitakayokidhi mahitaji ya watu 5,000 kwa miezi mitatu.

Mwezi Disemba vikosi vya jeshi la Iraq viliutwaa mji ulioko katika jimbo la Salah al-Din kutoka kwa

wanamgambo wanaotaka kuweka dola la Uislamu wenye msimamo mkali, ISIL ambao walikuwa wamedhibiti eneo hilo kwa kipindi cha miezi sita, na kwa hiyo kuzuia hatua ya mapema ya kuingilia kati au kufanya tathmini.

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, kuwasili kwa wakimbizi wanaokimbia baridi kali kumesababisha hali ya wakimbizi wa ndani na jamii wenyeji kuzorota

Inakadiriwa familia 1, 200 zinahitaji usaidizi wa haraka mathalan chakula, malazi, na vifaa vya matibabu, wengi wao wakiwa katika eneo la Dhuluiya na wakimbizi wa ndani kutoka Wilaya ya Al Alam