Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Saratani haisababishwi na bahati mbaya tu, yasema IARC

Saratani haisababishwi na bahati mbaya tu, yasema IARC

Shirika la Kimataifa la Utafiti kuhusu Saratani, IARC, limekanusha vikali madai ambayo yalichapishwa katika jarida la Sayansi mnamo Januari 2 na Dkt. Cristian Tomasetti na Dkt. Bert Vogelstein, wakisema kuwa aina nyingi za saratani ya wanadamu zinatokana na bahati mbaya tu.

Ripoti hiyo ilidai kuwa mazingira na mitindo ya maisha huchangia chini ya thuluthi moja ya visa vyote vya saratani. Ripoti hiyo, ambayo imepewa umaarufu mkubwa na vyombo vya habari, imedai kuwa kubadilika kwa chembechembe za mwili au bahati mbaya ndicho chanzo kikubwa cha saratani kwa ujumla kuliko sababu za urithi au kimazingira, na hivyo kupendekeza kuzingatia upimaji na ugunduzi wa mapema badala ya kuzuia kwa saratani.

IARC, ambacho ni kitengo maalum cha Shirika la Afya Duniani kinachohusika na utafiti katika saratani, kimesema kuwa iwapo ripoti hii itaeleweka vibaya, basi huenda ikawa na athari mbaya mno kwa utafiti katika saratani na mitazamo ya umma kuhusu afya.

Mkurugenzi wa IARC, Dkt. Christopher Wild amesema, ingawa inafahamika tayari kuwa kwa kiwango fulani, kuibuka kwa aina fulani ya saratani katika mwili wa mtu ni kitendo cha kubahatisha, hili halionyeshi kiwango kamili cha hatari ya saratani miongoni mwa watu. Kwa hiyo, amesema kuhitimisha kuwa bahati mbaya ni chanzo kikubwa cha saratani ni kupotosha watu, na hivyo huenda kukalegeza juhudi za kutambua vyanzo vya ugonjwa huo na kuuzuia.