Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Unyafuzi wapatiwa muarobaini Yemen, tusibweteke: OCHA

Unyafuzi wapatiwa muarobaini Yemen, tusibweteke: OCHA

Idadi ya watoto wenye utapiamlo uliokithiri, au unyafuzi nchini Yemen imepungua kwa asilimia 16 mwaka jana na kufikia watoto 840,000, kwa mujibu wa takwimu za  makadirio ya lishe nchini humo.

Ofisi ya Umoja wa Mataifa inayohusika na usaidizi wa kibinadamu, OCHA imesema mafanikio hayo yanatokana na misaada iliyotolewa ya kuwezesha kupanua wigo wa mipango ya usaidizi dhidi ya unyafuzi.

Hata hivyo OCHA imesema kuna hatari mafanikio hayo yakatumbukia nyongo iwapo misaada itapungua ikisema unyafuzi umejikita zaidi maeneo ya Kusini-Magharibi na pwani nchini Yemen.

Changamoto kubwa kwenye maeneo hayo ni ukosefu wa uelewa kuhusu unyonyeshaji wa watoto wachanga, uhaba wa maji safi na salama, matukio ya mara kwa mara ya magonjwa ya kuambukiza na ukosefu wa huduma za afya na lishe.

Usaidizi kwa Yemen ulipungua kwa asilimia 15 mwaka jana ambapo wahisani walitoa dola Milioni 335 ikilinganishwa na dola Milioni 396 mwaka 2013.