Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNESCO yaanzisha mjadala kuhusu uhuru wa kujieleza

UNESCO yaanzisha mjadala kuhusu uhuru wa kujieleza

Kuanzia leo Jumatano, Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni UNESCO linaongoza mjadala kuhusu ukatili dhidi ya waandishi wa habari, na umuhimu wa kutunza uhuru wa kujieleza.

Mazungumzo hayo ambayo yatafanyika mjini Paris, Ufaransa, yameandaliwa baada ya mashambulizi yaliyotokea dhidi ya gazeti linalotoa habari za kukejeli la Charlie Hebdo, na duka la Kosher, mjini Paris, ambapo watu 17 wamepoteza maisha.

Mkurugenzi Mkuu wa UNESCO Irina Bokova atafungua rasmi kikao hicho, ambako waandishi wa habari kutoka maeneo mbalimbali ya dunia watazungumza, pamoja na wawakilishi wa dini zote, hapo akisema:

(Sauti ya Bokova)

"Mashambulizi dhidi ya Charlie Hebdo yalikuwa mashambulizi dhidi ya uhuru wa kujieleza. Mabalozi wa dira hii ni waandishi. Takwimu zinashtua. Kila siku saba, mwandishi mmoja wa habari anauawa kwa sababu ya kufanya kazi yake na visa tisa kati ya kumi haviwajibishwi kisheria, na hilo halikubaliki. Kama shirika la Umoja wa Mataifa lenye jukumu la kutunza uhuru wa magazeti na wa kujieleza, UNESCO inasimama na kila mwandishi akiuawa na kuomba sheria itekelezwe."

Irina Bokova, ambaye ameshiriki katika maandamo ya kihistoria yaliyofanywa na watu milioni 1.5 na viongozi kutoka nchi 40 tofauti, mjini Paris, jumapili tarehe 11, ametoa wito wa kuchukua hatua dhidi ya ukatili na maneno ya ubaguzi, akisema UNESCO itaendelea kuendeleza uhuru wa kujieleza na kupigania usalama wa waandishi wa habari akisisitiza umuhimu wa kukuza elimu na maelewano baina ya mila na dini, na kujenga misingi ya amani katika mawazo ya watu.