Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Bado kuna kazi nyingi ya kufanya tangu tetemeko la ardhi Haiti- Ban

Bado kuna kazi nyingi ya kufanya tangu tetemeko la ardhi Haiti- Ban

Leo Januari 12 Umoja wa Mataifa unaadhimisha miaka mitano tangu tetemeko la ardhi lililotokea nchini Haiti mnamo mwaka 2010, ambapo watu zaidi ya 230,000 walifariki dunia wakiwemo wahudumu 102 wa Umoja wa Mataifa. Joshua Mmali ana maelezo zaidi

Taarifa ya Joshua

Mbali na maelfu ya vifo, tetemeko la ardhi nchini Haiti lilisababisha uharibifu mkubwa na kuwalazimu watu zaidi ya milioni 2 kuhama makwao.

Katika kuadhimisha siku hii, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon amesema kuwa kazi ya kuikwamua Haiti haijawa rahisi, akiongeza kuwa bado kuna kazi nyingi ya kufanya.

Katibu Mkuu amesema leo ni siku ya kuwaenzi watu waliofariki dunia katika tetemeko hilo, lakini pia ni wakati wa kuwakumbuka walionusurika na ambao uwezo wao kuhimili maafa hayo ni chanzo cha kuupa ubinadamu moyo.

Ban amesema harakati za kuikwamua Haiti zimekumbwa na changamoto nyingi, na kwamba bado kuna kazi nyingi ya kufanya ili kuhakikisha kuwa kuna ustawi wa kisiasa na taasisi za taifa, pamoja na utawala na maendeleo endelevu,

ujumbe ambao umesisitizwa na Jenerali Jose Luiz Jaborandy Junior Kamanda wa vikosi vya Ujumbe wa Umoja wa Mataifa Haiti, MINUSTAH.

“Tupo hapa, bega kwa bega na watu wa Haiti na mamlaka ya taifa kuunganisha yaliyopita nay a siku zijazo, tukitazamia yale yatakayowanufaisha watu wa Haiti.”