Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watoto wazidi kuathiriwa na machafuko Nigeria: UNICEF

Watoto wazidi kuathiriwa na machafuko Nigeria: UNICEF

Wakati machafuko yakizidi kuripotiwa Kaskazini Mashariki mwa Nigeria, shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF, limesema dunia inapaswa kuguswa na kile kinachoendelea nchini humo na kuchukua hatua. Taarifa zaidi na Joseph Msami

(TAARIFA YA MSAMI)

Katika taarifa yake Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF Anthony Lake amesema kuendelea kwa machafuko nchini humo kunaathiri watoto wasio na hatia akitolea mfano wa watoto , wanawake na vikongwe  takribani 2000 wameripotiwa kufanyiwa vitendo vya kinyama huko Baga.

Lake amesema kuwa kadhalika mtoto mwingine alifariki dunia baada ya bomu kumlipukia kifuani huko Maiduguri.

Mkuu huyo wa UNICEF ameitaka jumuiya ya kumataifa kutosahau  kuwa bado watoto zaidi ya 200 ambao walitekwa nyara na kundi la kigaidi la Boko Haram hawajapatikana.

Lake amesema maneno matupu hayatoshi kuelezea hasira dhidi ya vitendo hivyo wala kupunguza uchungu wa madhila hayo kaskazini mwa Nigeria na kusisitiza kuwa tasirwa za hivi karibuni nchini humo na athari zake kwa mustakabali wa taifa hilo zinahitaji hatua za haraka.