Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban Ki-moon akaribisha maandamano ya Paris

Ban Ki-moon akaribisha maandamano ya Paris

Baada ya mashambulizi ya kigaidi yaliyotokea dhidi ya gazeti la Charlie Hebdo, Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa amekaribisha maandamano yaliyofanyika mjini Paris, Ufaransa, Jumapili hii, kwa ajili ya kukumbuka waliokufa katika tukio hilo na wahanga wote wa ugaidi duniani, akisema kwamba ameguswa sana na picha za maandamano yaliyofanyika duniani kote.

Mjumbe Maalum wa Katibu mkuu Staffan de Mistura amewakilisha Umoja wa Mataifa katika maandamano hayo.

Katika taarifa iliyotolewa na msemaji wake, Ban Ki-moon ameongeza kutuma salamu zake za rambirambi kwa familia za wahanga, wakiwemo waandishi wa habari wa Charlie Hebdo, polisi waliouawa na watu waliokufa kwenye shambulizi dhidi ya duka la kosher.

Amesisitiza kwamba Umoja wa Mataifa unajitahidi kupambana na ugaidi duniani kote, kupigana ubaguzi dhidi ya wayahudi na watu wowote, na kutunza uhuru wa kujieleza wazi.

Katibu mkuu ameomba kuongeza bidii ili kuendeleza uvumilivu na maelewano. Amesema dunia inapaswa kupambana na ukatili wa kigaidi kwa njia inayoheshimu haki za binadamu.

Halikadhalika Ban ameonya dhidi ya ulipizaji kisasi unaolenga waislamu, akisema vitendo kama hivyo vitasaidia tu magaidi na kuchangia katika kuongeza ukatili.