Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Canada kupokea wakimbizi 13,000, UNHCR yaomba msaada kutoka nchi zingine

Canada kupokea wakimbizi 13,000, UNHCR yaomba msaada kutoka nchi zingine

Canada imeahidi kupokea wakimbizi 13,000 kutoka Syria na Iraq, kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi, UNHCR, baada ya Mkuu wa shirika hilo, Antonio Gueterres, kutoa ombi la kuwapatia hifadhi wakimbizi 100,000.

Msemaji wa UNHCR Adrian Edwards amesema tangazo la Canada ni mfano mzuri kwa nchi jirani za Syria zinazokabiliana na changamoto kadhaa wakiwa wanapokea idadi kubwa ya wakimbizi.

Tunadhani ni muhimu sana nchi zingine zianze kutoa nafasi ya kupokea wakimbizi kwa sababu watu wanazihitaji, na pia kuonyesha nchi jirani za Syria yenyewe kwamba msaada wa kimataifa upo. Kuna shinikizo kubwa juu ya kimbilio, na tunakaribia kufikia mkwamo kwenye baadhi ya maeneo. Ndio maana ni muhimu kuwapatia suluhu watu ambao wanakimbia makwao ili kuokoa maisha yao

Ahadi za Canada zinafuata maamuzi ya Lebanon ya kuongeza masharati dhidi ya upokeaji wa wakimbizi kutoka Syria, wakati idadi yao imeshafika milioni 1.5 nchini humo.

Takwimu za Umoja wa Mataifa zinaonyesha kwamba idadi ya wakimbizi kutoka Syria imefika milioni 3.2, wengine milioni 7 wakiwa wakimbizi wa ndani.