Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza la Usalama lalaani shambulizi la kigaidi Yemen

Baraza la Usalama lalaani shambulizi la kigaidi Yemen

Wanachama wa Baraza la Usalama wa Umoja wa Mataifa wamelaani vikali shambulizi lilolotokea jumatano leo, ambapo angalau watu 37 waliuawa, wakiwemo wafanyakazi wa serikali, baada ya bomu kulipuliwa katika chuo cha polisi, mjini Sana’a, nchini Yemen.

Katika taarifa iliyotolewa leo, baraza hilo limelaani pia mashambulizi yaliyotokea awali mwezi huu mjini Dhamar, na mjini Ibb tarehe 31, Disemba, nchini humo.

Wanachama pia walituma salamu za rambirambi kwa familia za wahanga na serikali ya Yemen, huku wakisistiza kwamba ugaidi ni tishio kubwa kwa usalama na amani ya kimataifa, na hauwezi kuthibitishwa kwa msingi wowote.

Halikadhalika, wanachama wa baraza hilo wamesisitiza watekelezaji wa uhalifu huo wachukuliwa hatua za kisheria, pamoja na waandaji na wafadhili wao, wakiziomba nchi zote kushirikiana na Yemen ili kufanikisha hilo, kwa kuheshimu sheria ya kimataifa ya haki za binadamu katika vita hivi dhidi ya ugaidi.

Aidha, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amelaani mashambulizi hayo akiwaomba raia wa Yemen wote kuungana katika kupambana na ugaidi ili kuleta utulivu na usalama nchini humo.