Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wahamiaji zaidi waokolewa baharini Mediterenia

Wahamiaji zaidi waokolewa baharini Mediterenia

Dunia ikiwa imeadhimisha siku ya wahamiaji hivi karibuni, maelfu ya wahamiaji waliokuwa wanajaribu kuvuka kupitia bahari ya Mediterenia kuingia nchini Italia kwa meli mbili wameokolewa na maafisa wa shirika la kimataifa la uhamiaji IOM. Taarifa zaidi na Abduilahi Boru.

(TAARIFA YA BORU)

Taarifa ya IOM inasema kuwa manusura wa tukio hilo wamewaambia maafisa wa IOM kuwa wasafirishaji haramu waliwatosa baharini wanawake , wanaume na watoto bila kujali kuwa wangeweza kuzama.

IOM inasema kuwa mathalani meli ya Moldova aina ya Blue sky M iliyobebea watu zaidi ya mia saba ilionekana ufukweni usiku wa kuamkia mwaka mpya wa 2015 katika eneo liitwalo Apulia nchini Italia ambapo maafisa walibaini makumi ya raia wa Syria waliosema walisafiri kwa takribani wiki moja na kulipa hadi dola 6000 kwa wasafirishaji haramu wa Uturuki.

Joel Millman ni msemaji wa IOM..

(SAUTI)

"Hizi ni meli kubwa kwenye bahari na makundi madogo ya wahamiaji wanasafiri na wanachukua hadi wiki moja kujaza shehena na kama hii ina maanisha kwamba wanakotoka hakuna mamlaka zinazoweza kubaini taarifa za meli tunahoji ni vipi wanaweza kuendeleza shughuli zao."

IOM imetaka juhudi za jumuiya ya kimataifa katika kupambana na usafirishaji haramu wa wahamiaji .